ELCT North Eastern Diocese
Koteti yapata usajili sasa kuanza udahili
- Details

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Dkt. Msafiri Joseph Mbilu ameipongeza Bodi inayosimamia Zahanati ya Mtae Mission pamoja na Washarika wa Usharika huo kwa juhudi walizozifanya na kupelekea zahanati hiyo kufunguliwa tena kwa upya


ambayo itakwenda kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa eneo.


ASKOFU DKT. MBILU AKIKATA UTEMBE ISHARA YA UZINDUZI WA MNARA WA KENGELE USHARIKA WA MTAE MTAA WA MAMBO
Pongezi hizo amezitoa leo akiwa katika Jimbo la Kaskazini Usharika wa Mtae kwenye Ibada ya Jumapili iliyokuwa na matukio mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa Mnara wa kengele katika Usharika wa Mtae Mtaa wa Mambo,kufunguliwa kwa Upya Zahanati ya Mtae pamoja na tendo la kuwabariki vijana wa kipaimara ambapo amesema zahanati hiyo ni Muhimu kwa wanamtae na kuipongeza bodi hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Aidha Askofu Dkt. Mbilu amesema kufunguliwa kwa upya zahanati hiyo ni kutunza heshima ya Usharika wa Mtae na Dayosisi kwa ujumla, na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya Afya katika eneo hilo ambapo awali wananchi walilazimika kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Wilaya Lushoto.

Kadhalika Askofu Dkt. Mbilu amesema azma ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ni pamoja na kutoa huduma za kiroho na za kimwili ikiwemo zahanati hiyo iliyoanzishwa mwaka 1926 kuwahudumia watu wote tena kwa upendo pindi wanapofika kupatiwa matibabu na hivyo kuitaka bodi ya zahanati hiyo kutokuwa sababu yoyote itakayo pelekea kufungwa tena kwa zahanati hiyo.Katika Ibada hiyo jumla ya vijana wapatao 90 wamebarikiwa na watatu kati yao kubatizwa.


Katika Hatua Nyingine Askofu Dkt. Mbilu ametoa wito kwa wazazi, walezi na watu wote wanaopenda kujiunga na kozi ya Pharmacy katika ngazi ya Certificate na Diploma kwenye Chuo cha Kolowa Technical Training Institute chenye usajili namba KOTETI/HAS/249, kutuma maombi kwa kupitia mfumo wa (CAS) kwenye tovuti ya NACTE ambapo dirisha la awamu ya pili la Udahili wa pamoja kwa kozi za Afya litafunguliwa hapo kesho tarehe 15 Agosti,2022.

Chuo hiki kipo Wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga na kitatumia majengo ya kilichokuwa Chuo Kikuu cha SEKOMU.


- Hits: 14895
Askofu Dkt. Mbilu awataka Wachungaji kusimama imara kukemea mafundisho potofu ya neno la Mungu.
- Details

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewataka wachungaji kusimama imara ili kupinga na kukemea mafundisho potofu ya neno la Mungu yanayoletwa na watumishi wa uongo maeneo mbalimbali nchini.

Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo leo tarehe 07/08/2022 akiwa katika Jimbo la Pwani Usharika wa Kana kwenye Ibada ya kubarikiwa na kuingizwa kazini kwenye huduma ya Kichungaji, Mch. Jonathan Denis Hizza na kusema kuwa katika nyakati tulizonazo kumejaa mafundisho ya uongo kutokana na watu mbalimbali ambao wameibuka na kujiita watumishi wa Mungu.

Amesema kuwa watumishi hao hawajaandaliwa katika utaratibu wa kumtumikia Mungu bali wamejiandaa wenyewe jambo ambalo linasababishwa na ukosefu wa ajira hivyo kupelekea mtu anaamua kuvamia Biblia kwa madai ya kufunuliwa na kuanza kufundisha na kupotosha jamii.

Aidha amemtaka Mchungaji Jonathani Hiza kutambua kuwa ameitwa katika wakati mgumu ambao Kanisa limekumbwa na mafundisho hayo hivyo anapaswa kupinga mafundisho hayo na kuongeza kuwa mchungaji yeyoto ambaye hatokemea mafundisho hayo potofu hafai kwa kazi ya Mungu.

Sambamba na hayo amemkumbusha Mch. Jonathan Hiza kutambua ameitwa kuwatumikia watu wote bila kuwa na makundi katika Kanisa la Mungu huku akimtaka kujishughulisha na miradi mbalimbali ya kiuchumi.

Sehemu ya Washarka wa Usharika wa Kana
- Hits: 13842
Askofu Dkt. Fedrick Shoo atoa rai juu ya Kiwanda cha Vuga Press
- Details

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Askofu Dkt. Fedrick Shoo ametoa rai kwa Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu kuendeleza jitihada za kukifanya Kiwanda cha uchapishaji cha Vuga Press Publishing House ambacho kihistoria ni cha kwanza kwa uchapishaji Afrika Mashariki kiendelee na uzalishaji.

Mkuu wa Kanisa ameyasema hayo leo tarehe 02/08/2022 akihitimisha ziara yake katika kiwanda hicho kinacho milikiwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na kuongeza kuwa kuzingatia historia ya kiwanda hicho na mchango wake katika machapisho jitihada za kupata mashine na mitambo ya kisasa ziendelee kuwepo kwani uwitaji bado ni mkubwa.

Kwa upande wa meneja wa kiwanda hicho Mch. Moses Shemweta amemuelezea mkuu wa KKKT kuwa kiwanda hicho cha uchapaji wa maandiko kilianzishwa mwaka 1912 na wamisionari kutoka Ujerumani katika eneo la Vuga Mission mahali ambapo sasa ni Chuo cha Biblia na Kituo cha Mikutano Vuga. Ameongeza kuwa mwaka 1949 kutokana na changamoto ya miundo mbinu ya barabara na umeme kiwanda hicho kilihamishiwa katika eneo la Soni.

Meneja wa kiwanda cha Vuga Press Mch. Moses Shemweta

Kiwanda cha Vuga Press kilianzishwa hasa kwa kusudi la kuchapa maandiko mbalimbali ya makanisa, japo baadae kilihusika katika kuchapa maandiko ya Serikali hasa miaka 15 ya kwanza baada ya Nchi ya Tanzania kupata uhuru hadi pale Serikali ilipoanzisha kiwanda chake na kuchukua baadhi ya watumishi kutoka kiwandani hapo.

Pamoja na Uchapaji, kiwanda hicho kilikuwa kiwanda pekee kilichotoa mafunzo ya uchapaji (Printing School) ya uhakika kwa vijana wengi hapa Nchini, hadi pale Serikali ilipoanzisha mafunzo hayo katika chuo cha VETA Dar es salaam pia ikitumia wataalamu kutoka Vuga Press. huku katika kiwanda cha Vuga Press mafunzo hayo yalikoma mwaka 2010.

Aidha kiwanda hicho ndipo ilipokuwa ofisi ya maandiko ya KKKT, kabla haijahamishiwa Arusha. Kwa wakati huu wateja wakubwa wa kiwanda hicho ni Dayosisi yenyewe, makanisa mengine, mashirika na taasisi za serikali na watu binafsi ndani na nje ya mkoa wa Tanga.

Vuga Press inaundwa na idara kuu mbili ambazo ni Utawala na Uzalishaji. Utawala: Idara hiyo inahusika na uongozi wa kituo, uhasibu, ukadiriaji wa gharama na masoko. Uzalishaji: Idara hii ina sehemu kuu tatu ambazo ni: -Uandaaji – Composition and Designing. Uchapaji.Ujaladiaji na umaliziaji.

KATIBU MKUU KKKT-DKMs MCH. GODFREY TAHONA WALALAZE
Vuga Press kama kitega uchumi cha Dayosisi imekuwa ikichangia katika pato na kazi ya Misioni na Uinjilisti ya Dasosisi tangu kilipoanzishwa. Pamoja na kuchangia bajeti ya Dayosisi, kiwanda hicho kilishiriki kikamilifu katika kujenga majengo ya Ibada kwenye maeneo ya misioni ya Masaini, Ununuzi wa kituo cha Martin Luther Garden – Segera pamoja na ujenzi hoteli ya Tumaini Lushoto.

Uongozi wa kiwanda hicho umeushukuru uongozi wa KKKT – Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa jitihada kubwa na mipango mbalimbali kuhakikisha kituo hicho kinaendelea kuwepo kwa kukijengea uwezo kwa upya, na wanaunga mkono jitihada hizo kwa kutimiza vyema majukumu yao ya kila siku ili kiwanda hicho kiimarike na kuwa na tija kwa Kanisa.

Awali kabla ya msafara wa Mkuu wa KKKT kufika katika kiwanda hicho Mkuu wa KKKT Dkt. Fredrick Onael Shoo aliagana na uongozi wa KKKT – Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, wafanyakazi wa Ofisi Kuu katika Ofisi za Makao Mkuu ya Dayosisi.


- Hits: 14054
Askofu Dkt. Shoo awaasa wanafunzi Shule ya Sekondari Lwandai
- Details

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Askofu Dkt. Fredick Onael Shoo amewaasa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Lwandai inayomilikiwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kusoma kwa bidii na kumtanguliza Mungu katika masomo yao ili kutimiza ndoto zao.

Ameyasema hayo leo tarehe 01/08/2022 akihitimisha ziara yake ya siku 6 ndani ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki katika Jimbo la Kaskazini wakati wa ufunguzi wa maabara ya kujifunzia masomo kwa vitendo ambayo imefanyiwa ukarabati mkubwa katika Shule ya Sekondari Lwandai, huku akifurahishwa na matokea mazuri na kuahidi kuwa balozi wa Shule hiyo.

Askofu Dkt. Shoo pia ameupongeza uongozi wa Dayosisi chini ya Askofu Dkt. Joseph Mbilu, kwa jitihada mbalimbali zilizofanywa na uongozi kwa kuanza kurudisha uhai katika Shule hiyo hivyo kuwa na matumaini kuwa shule hiyo itakuwa ni moja ya Shule bora kitaifa.


Kwa upande wake Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Dkt Msafiri Joseph Mbilu amesema kuwa Mlalo ndio kitovu cha Dayosisi na kusisitiza kuwa wapo watumishi mbalimbali ambao wamezaliwa na wengine kutumika katika Usharika wa Mlalo sambamba na kusema kuwa Shule ya Lwandai imekuwa na historia kubwa kwakuwa ndipo ilipoanzia Shule ya Sekondari Eliboru na Chuo kikuu cha Makumira.

Nae Mbunge wa Jimbo la Mlalo Mhe. Rashidi Shangazi ameahidi kushirikiana na Kanisa katika mambo mbalimbali yanayohitaji msaada kutoka serikalini ili kupata msaada wa haraka sambamba na kushukuru Kanisa kwa kutoa huduma muhimu kwa jamii ikiwemo mashule Hospitali na vituo vya huduma ambavyo kipekee vinamilikiwa na Kanisa.

Ikumbukwe kuwa ziara ya mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluther Tanzania katika Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ilianza tarehe 27/7/2022 na kuhitimishwa tarehe 01/08/2022 ambapo katika ziara hiyo ametembelea sharika na vituo mbalimbali vya huduma pamoja na kuweka mawe ya msingi katika Sharika za Dayosisi. Hapo kesho Mkuu wa KKKT atapata nafasi ya kuagana na mwenyeji wake Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu ndipo atakapo rejea katika majukumu yake.



- Hits: 15955
Page 75 of 137

