ELCT North Eastern Diocese
ASKOFU KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI MASHARIKI AZINDUA BODI YA MFUKO WA PENSION
- Details
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki. Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, leo tarehe 04 Machi 2026, amezindua rasmi Bodi ya Mfuko wa Pension iliyochaguliwa na Halmashauri Kuu ya Dayosisi.
Baada ya uzinduzi huo, Bodi ilifanya kikao chake cha kwanza katika Kituo cha Mbuyukenda, mkoani Tanga.
Akizungumza katika hafla hiyo, Baba Askofu alieleza kuwa mfuko huo umeanzishwa kwa ajili ya kuhakikisha mustakabali bora wa watumishi wa kiroho wanaolitumikia Kanisa. Alisisitiza kuwa mfuko huo unahitaji usimamizi imara, maono makubwa, na uwajibikaji wa hali ya juu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Alifafanua kuwa jukumu kuu la Bodi hiyo ni kuhakikisha watumishi wa kiroho walioitumikia Dayosisi wanatunzwa na kupongezwa ipasavyo pindi wanapostaafu utumishi wao. Aidha, aliitaka Bodi kutoa elimu kwa Wakristo wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kuhusu umuhimu wa Mfuko wa Pension na kuhamasisha ushiriki wao kikamilifu.
Baba Askofu aliongeza kuwa masuala ya watumishi yanapowekwa mikononi mwa waumini, kupitia vipawa vyao na moyo wao wa kujitoa, yanaweza kuleta mafanikio makubwa katika kuwahudumia na kuwajali watumishi wa Kanisa.
Kwa upande wake Mwenyekiti Bw. Dickson Mosi, mara baada ya kupokea wajibu huo ameahidi kutumia vipawa na utaalamu wao kubuni vyanzo vipya vya mapato, kuboresha vilivyopo, pamoja na kusimamia Mfuko huo kwa uadilifu na uwazi kwa manufaa ya Dayosisi na watumishi wake.

- Hits: 41
Taarifa Ziara ya Botswana kwenye Mkutano wa UEM Kanda ya Afrika
- Details
Dayosisi yetu imepata heshima kubwa ya kushiriki katika Mkutano wa Kanda ya Afrika ulioandaliwa na United Evangelical Mission (UEM), uliofanyika katika mji wa Gaborone, nchini Botswana kuanzia tarehe 23 Februari hadi 1 Machi mwaka huu.
Katika mkutano huu muhimu dayosisi yetu imewakilishwa na viongozi na wajumbe wafuatao:
-
Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu
-
Mch. Happiness Diu – Mjumbe wa Bodi ya UEM Afrika anayewakilisha wanawake
-
Elvina Riziki – Mwakilishi kundi la vijana
Mkutano huu uliwakutanisha washiriki kutoka nchi mbalimbali za Afrika kwa lengo la kujadili masuala ya huduma, umoja, uinjilisti, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa makanisa yaliyo chini ya UEM. Ilikuwa ni nafasi ya kubadilishana uzoefu, kujifunza, na kupanga mikakati ya kuendeleza kazi ya Mungu.
Katika mkutano huo, Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu alipata fursa ya kuwa mnenaji wa Neno Kuu la UEM. Ujumbe wake ulijikita katika andiko kutoka Injili ya Mathayo 7:5 lisemalo: “Itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.”
Kupitia Neno hili, Baba Askofu alisisitiza umuhimu wa kujitathmini, toba, na unyenyekevu katika huduma na maisha ya kila siku. Aliwahimiza washiriki kuanza mabadiliko ndani yao kabla ya kuwakosoa au kuwaongoza wengine, akisisitiza kuwa uongozi wa kweli huanzia katika usafi wa moyo na nia njema.
Tunamshukuru Mungu kwa safari hii, uwakilishi mzuri wa Dayosisi yetu, na kwa mafanikio ya mkutano huu. Tunaamini kuwa matunda ya mkutano huu yataonekana katika kuimarika kwa huduma zetu na katika kukuza umoja wa Kanisa la Mungu barani Afrika na Duniani kote.

- Hits: 36
Askofu Dkt. Mbilu afungua Kikao Kazi cha Tathmini ya Mwaka 2025
- Details

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amefungua rasmi kikao cha tathmini kwa kazi zilizotekelezwa katika kipindi cha mwaka 2025.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika tarehe 12/02/2026 katika Hoteli ya Tumaini Mbuyukenda, Jijini Tanga, Askofu Dkt. Mbilu amesema kuwa lengo kuu la kikao hicho ni kuweka msingi imara kwa watumishi kutambua walipotoka, walipo na wanakoelekea katika utendaji wao wa kazi. Amesisitiza kuwa tathmini ni nyenzo muhimu katika kupima mafanikio, kubaini changamoto na kupanga mikakati madhubuti ya kuboresha utendaji kwa siku zijazo.
- Hits: 1163
Askofu Dkt. Mbilu akutana na kufanya mazungumzo na Helga Walter
- Details

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dkt. Msafiri Mbilu, alipata fursa ya kupokea ugeni wa kiongozi wa undugu Helga Walter kutoka Hainberg-Gymnasium Göttingen nchini Ujerumani.
Katika mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki tarehe 05/02/2026 , pande zote mbili zilijadili kwa kina namna ya kuendelea kuimarisha na kuboresha undugu uliopo kati yao, hususani katika nyanja za elimu na huduma za kijamii.
Aidha, Askofu Dkt. Mbilu alitumia fursa hiyo kutoa shukrani za dhati kwa Helga pamoja na wadau wengine wa maendeleo kutoka Hainberg-Gymnasium Göttingen kwa michango yao ya kimaendeleo, hususani katika Shule ya Sekondari Lwandai pamoja na vituo vya diakonia vilivyopo Irente vinavyomilikiwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.
Ziara hiyo ilionesha mshikamano na dhamira ya pamoja ya kuendeleza ushirikiano wenye tija kwa manufaa ya jamii.
- Hits: 1462
Page 1 of 136

