
Uongozi wa KKKT – Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ukiwakilishwa na Katibu Mkuu Mwl. Julius Madiga, umefanya hafla ndogo ya makabidhiano ya mradi wa maji (Mazi kwa Woshe) tarehe 10/03/2026 katika ofisi ya Afisa Tarafa-Mnazi.
Lengo kuu la hafla hiyo lilikuwa ni mkandarasi mjezi wa kampuni ya Ntama and faith company lmtd, kukabidhi rasmi mradi huo kwa Dayosisi, na baadaye Dayosisi kupitia Katibu Mkuu kukabidhi mradi kwa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) pamoja na Kamati ya Maji ya UMBAWASO kwa ajili ya uendeshaji na usimamizi wake.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Mwl. Julius Madiga alieleza kwa kina namna mradi huo ulivyopatikana kupitia ufadhili wa marafiki wa Dayosisi kutoka MAZI KWA WOSHE MINDEN – Ujerumani. Alifafanua kuwa utekelezaji wa awali ulisimamiwa na Idara ya Ujenzi na Ufundi ya Dayosisi kwa kushirikiana na mhandisi wa MAZI KWA WOSHE Mhandisi Godfrey Magalla, kabla ya kuendelezwa na mkandarasi chini ya usimamizi wa RUWASA.
Aidha, Katibu Mkuu alisisitiza umuhimu wa utunzaji wa miundombinu ya mradi huo, akibainisha kuwa huduma ya maji ni muhimu kwa maendeleo ya jamii na ustawi wa wananchi. Alieleza kuwa Kanisa linaendelea kutimiza wajibu wake wa msingi wa kumhudumia mwanadamu kiroho, kimwili na kiakili, na miradi kama hii ni sehemu ya ushuhuda wa huduma hiyo kwa jamii.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Dayosisi Bw. William Mwanga, alisisitiza umuhimu wa kuutunza mradi huo kwa kuwa ni mradi mkubwa uliosanifiwa na kujengwa kwa ubora wa hali ya juu ili uweze kudumu kwa vizazi na vizazi. Alielezea pia baadhi ya miundombinu mikubwa ya mradi huo ikiwemo tank la kuhifadhi maji lenye ujazo wa zaidi ya lita 200,000.
Naye Mwakilishi/Kaimu Meneja wa RUWASA, Bw. Fred Mbulumi, aliishukuru sana KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki chini ya uongozi wa Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu kwa kuanzisha ndoto hii njema ya kuwapatia huduma ya maji wananchi wa Mnazi na vijiji vya jirani. Pia aliiomba Dayosisi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo kwa jamii.
Kwa upande wake, Afisa Tarafa wa Tarafa ya Umba, Bw. Shadrack George Mwambene, amepongeza ushirikiano mkubwa ulioonyeshwa kati ya Kanisa na Serikali ambao umefanikisha utekelezaji wa mradi huu muhimu kwa wananchi.
Mradi huu unatarajiwa kuwa msaada mkubwa katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa eneo la Mnazi na maeneo ya jirani.

