MAKAYO KOROGWE: Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania - Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs) amewataka Wakristo kuacha kufuata mafundisho potofu na badala yake wachukue jukumu la kuyashuhudia Maandiko Matakatifu kwa wengine.
Akizungumza Alhamisi, Julai 31, 2025, wakati wa Ibada ya Kipaimara iliyofanyika katika Jimbo la Magharibi, Usharika Mteule wa Msomera, Mtaa wa Makayo, Askofu Dkt. Mbilu alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mmoja kushuhudia nuru ya kweli na upendo wa Yesu Kristo.
Askofu Dkt. Mbilu amewataka washarika wa Mtaa wa Makayo, ambao wengi wao ni jamii ya wafugaji wa Kimasai, kuacha kuwasikiliza watu wanaokwenda maeneo yao na kudai kuleta "nuru ya Wamasai," akisisitiza kuwa Yesu anatosha na yeye ndiye Nuru ya Ulimwengu. Aliwahimiza kuiga mfano wa Yesu Kristo, ambaye aliupenda ulimwengu wote na hakuja kwa ajili ya Wamasai pekee bali kwa ajili ya ulimwengu mzima.
Katika Ibada hiyo ilitanguliwa na ufunguzi wa Kanisa la Usharika Mteule wa Msomera, Mtaa wa Makayo. Jumla ya vijana 64 walibarikiwa na walichangia Tsh. 310,000 na mara baada ya kuungwa mkono na wanaume na wanawake waliohudhuria Ibada hiyo, jumla ya shilingi 585,000 zilipatikana na zitaelekezwa katika ulipaji wa deni la Dayosisi.
Tufuatilie kwenye mitandao yetu ya kijamii