Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu yupo katika ziara ya kikazi Nchini Poland ambapo anahudhuria mkutano wa kamati ya Ibada na Muziki ya Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani (LWF) unaofanyika kwenye mji wa Krakow kwaajili ya kuandaa Mkutano Mkuu utakaofanyika Nchini Poland mwaka 2023.
Kamati hii imeundwa mwaka 2021 na ofisi ya Katibu Mkuu wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani ambayo makao makuu yake yapo Geneva Uswis. Kamati hii ina wajumbe kumi kutoka Ujerumani,Canada,Norway,Hungary,Poland,Hong Kong,USA,Brazil,Switzeland na Africa ambapo mjumbe muwakilishi ni Askofu Dkt. Msafiri Mbilu.
Akiwa katika ziara ya kikazi Nchini humo Askofu Dkt. Mbilu aliongoza Ibada ya chakula cha Bwana katika Usharika wa Kanisa la Kilutheri ulioko kwenye Mji wa Krakow Jumapili tarehe 13.03.2022.
Pia amepata wasaa wa kukutana na Bi. Salome Mmaka binti wa Mch. Yohana Mmaka ambaye ni mwana Dayosisi wa KKKT-DKMs ambaye ni mwanafunzi kwenye Chuo Kikuu cha Kharkiv Aviation Institute kilichopo Nchini Ukraine ambapo anasomea kozi ya Aerospace Engineering.