Naye atafuta kila chozi katika macho yao,wala mauti haitakuwepo tena,wala kilio,wala maumivu hayatakuwepo tena, kwa kuwa mambo ya kwanza , yamekwisha kupita UFUNUO 21:4.
Msaidizi wa Askofu,KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch. Michael Mlondakweli Kanju,leo tarehe 12/03/2022 ameshiriki Ibada ya mazishi ya Bibi Neema Silas Jengo iliyofanyika katika Usharika wa Makorora Jimbo la Pwani.
Marehemu Bibi Neema Jengo aliitwa mbinguni alfajiri ya tarehe 10/03/2022 nyumbani kwake Makorora Tanga na amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 89, katika uhai wake alikuwa ni mke wa Mchungaji Silas Mathayo Kakoto ambaye pia alishaaitwa mbinguni mnamo tarehe 13/12/2004.
Hata hivyo marehemu Bibi Neema katika uhai wake aliwahi kuwa mwalimu wa Shule ya Jumapili katika Sharika mbalimbali walizowahi kutumika yeye na mume wake.
Mwili wa Bibi Neema umepumzishwa katika makaburi ya familia yaliyopo katika Kijiji cha Vunde Manyinyi Wilaya ya Mkinga Mkoa wa Tanga.
Kwa niaba ya Uongozi wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kupitia kwa Msaidizi wa Askofu Mch. Michael Mlondakweli Kanju ambaye alimuwakilisha Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu kwenye Ibada hiyo ya kuaga na mazishi amesema kuwa, Uongozi unatoa pole kwa familia ya marehemu, watumishi wote wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki , ndugu jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huo mzito. Mungu awape nguvu na faraja ya kweli katika kipindi hiki kigumu.
Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe.