![]()
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dkt. Msafiri Mbilu, leo tarehe 05/05/2026 amefanya ziara ya kikazi katika Shule ya Bishop Jali Lutheran Junior Seminary, yenye lengo la kukagua na kujionea hali ya miundombinu pamoja na maendeleo ya kitaaluma shuleni hapo.
Akizungumza na walimu na wanafunzi, Askofu Dkt. Mbilu amesisitiza umuhimu wa kuenzi misingi iliyowekwa na viongozi wa Dayosisi waliopita akiwemo Hayati Joseph Mathayo Jali kuendelea kutiana moyo ili kuhakikisha yale yaliyoyanzishwa yanaendelezwa kwa mafanikio zaidi.
Katika hatua nyingine, Askofu Dkt. Mbilu ametoa pole kwa jumuiya ya shule hiyo kufuatia kifo cha aliyekuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo Mwl. Mwanga kilichotokea mwaka jana huku akiwahimiza kubaki imara na kuendelea kushirikiana katika kujenga mustakabali wa shule hiyo.
Aidha, Askofu Dkt. Mbilu amewapongeza walimu na wanafunzi kufuatia matokeo mazuri ya kitaaluma, hususani wanafunzi waliofaulu kwa daraja la pili na la tatu, akisisitiza kuwa kwa kuongeza juhudi katika masomo, shule hiyo ina uwezo mkubwa wa kufika mbali zaidi kitaaluma.
Kwa upande wa maendeleo ya miundombinu, Askofu Dkt.Mbilu amesema Dayosisi inaendelea kutafuta njia bora za kuboresha mazingira ya kujifunzia. Pamoja na uwepo wa maji Askofu Dkt. Mbilu ameahidi kusaidia upatikanaji wa maji ya uhakika kwa kununua pampu ya kisima ambacho kishaa chimbwa pamoja na matanki mawili ya kuhifadhia maji ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji wakati wote.
Sambamba na hilo, Askofu Dkt.Mbilu ameahidi kulifanyia kazi suala la usafiri kwa kuangalia uwezekano wa kutoa gari moja liliyopo katika Ofisi Kuu ya Dayosisi ili liweze kupelekwa shuleni hapo ndani ya wiki ijayo kwa ajili ya kuwahudumia walimu na wanafunzi.
Katika jitihada za kuboresha elimu ya TEHAMA, Askofu Dkt. Msafiri Mbilu amemuelekeza Afisa TEHAMA, wa Dayosisi Amasia Shemkala, kufuatilia upatikanaji wa kompyuta tano pamoja projector na Printer, ili kuimarisha mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji katika shule husika.
Hatua hii ya Baba Askofu inaonesha kwa vitendo umuhimu mkubwa wa TEHAMA katika sekta ya elimu. Kupitia matumizi ya teknolojia, walimu wanaweza kufundisha kwa njia shirikishi na yenye mvuto zaidi, huku wanafunzi wakipata fursa ya kujifunza kwa vitendo na kujiandaa kukabiliana na mahitaji ya dunia ya kisasa inayotegemea teknolojia.
Aidha, upatikanaji wa vifaa hivi utasaidia kuongeza ufanisi wa ufundishaji, kupanua wigo wa maarifa kwa wanafunzi, na kukuza ubunifu pamoja na stadi za kidijitali ambazo ni muhimu katika soko la ajira la sasa na la baadaye. TEHAMA si nyenzo ya ziada tena, bali ni hitaji la msingi katika kuhakikisha elimu bora na jumuishi inapatikana kwa wote
Katika ziara hii Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, aliambata na Mkurugenzi wa Huduma za Jamii Mwl. Afizai Vuliva.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Jamii KKKT-DKMs ametoa shukrani za dhati kwa Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu kufuatia ziara yake katika Shule hiyo ya Bishop Jali Lutheran Junior Seminary, akieleza kuwa uwepo wa kiongozi huyo ni faraja kubwa na chachu ya maendeleo katika taasisi hiyo.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mkurugenzi huyo amesema kuwa maelekezo na ushauri uliotolewa na Baba Askofu ni ya msingi katika kuboresha huduma za elimu na malezi kwa wanafunzi. Ameahidi kuyafanyia kazi kwa haraka na kwa umakini maelekezo yote yaliyotolewa, ili kuhakikisha shule inaendelea kuwa kituo bora cha malezi, taaluma na nidhamu.
Aidha, amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya uongozi wa Dayosisi na taasisi zake ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya kutoa elimu yenye viwango vya juu, akiahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo kwa ufanisi na uwajibikaji

