Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu ameongoza Ibada iliyokuwa na tendo la kuzindua Jimbo la tano ndani ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki,Ibada hiyo pia iliambatana na kuingizwa kazini kwa Mkuu wa Jimbo hilo Mch. Ishmael Reuben Ngoda pamoja na Katibu Mkuu wa Dayosisi Mwl. Julius Samwel Madiga .

Akizungumza katika Ibada hiyo iliyofanyika tarehe 08/10/2023 katika Usharika wa Handeni yalipo Makao Makuu ya Jimbo hilo, Askofu Dkt. Msafiri Mbilu amewataka viongozi hao walioingizwa kazini kumtanguliza Mungu katika utumishi wao kwani watakutana na mambo magumu.

“Ndugu zangu katika utumishi wenu jueni kwamba mtakutana na mambo makubwa na magumu ambayo hamkuwahi kuyaona ila msije mkakata tamaa, mtangulizeni Mungu aliyewaita katika utumishi wenu mlioitiwa.”

Awali Baba Askofu Dkt. Msafiri Mbilu akizindua Jimbo hilo alimkabidhi Mkuu wa Jimbo hilo gari kama ishara ya kuzindua Jimbo hilo na kusema kwamba anatarajia kuona maendeleo katika Jimbo hilo Jipya ikiwemo miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo itatekelezwa.

Askofu Dkt. Msafiri Mbilu alisema Jimbo hilo Jipya la Magharibi lina jumla ya Sharika  kumi (10) ambazo ni, Usharika wa Handeni (Makao Makuu ya Jimbo), Usharika wa Kwalukonge, Usharika Mteule Msomera, Usharika wa Eden Asilia Kilindi, Usharika wa Gombero, Usharika wa Misima, Usharika wa Kabuku, Usharika wa Kilindi, Usharika wa Mkata na Usharika wa Saunyi.

Jimbo Jipya la Magharibi limetokana na kugawanywa kwa Jimbo la Tambarare lilikuwa na jumla ya Sharika 23 na kupelekea kugawanywa kwa Jimbo hilo na ndipo Jimbo Jipya la Magharibi lilipo zaliwa, na hii ni kutokana na kazi ya Misioni kuendelea kukuwa katika eneo hilo. Kuzinduliwa  kwa Jimbo hilo Jipya kutasaidia kuwafikia Wakristo katika maeneo yao na kupata huduma mbalimbali za kiroho kwa wakati katika maeneo yao.

Naye Mkuu wa Jimbo Jipya la Magharibi Mch. Ishmael Reuben Ngoda, amemshukuru Baba Askofu Dkt. Msafiri Mbilu pamoja na Halmashauri Kuu ya Dayosisi kwa kumuamini na kumuona anafaa kuongoza Jimbo hilo katika nafasi ya Mkuu wa Jimbo huku akiahidi kufanya kazi kwa bidii na kwa uaminifu kwa kushirikiana na wana KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki katika kuitenda kazi ya Bwana.

Katika itikio lake Mkuu wa Jimbo la Magharibi, Mch. Ishmael  Ngoda ameongeza kwa kusema kuwa atasimamia mafundisho sahihi ya Neno la Mungu kwani nyakati hizi kumekuwa na upotoshaji juu ya mafundisho ya Neno la Mungu.

“Natambua nyakati tulizo nazo Kanisa linakutana na wimbi zito la mahubiri na mafundisho ya kila aina wamejitokeza watu wanaojiita watumishi mitume na manabii wanaofundisha na kuhubiri tofauti na ilivyo kweli ya Neno la Mungu, watu hawa wamegeuza shida,magonjwa na taabu za watu kuwa fursa ya kuwahadaa na kuwaibia mali zao kwa kutumia mistari ya Biblia.
Hivyo nitashirikiana na watumishi wenzangu kuhakikisha Wakristo wanatunzwa kiroho kwa njia ya mafundisho sahihi ya Neno la Mungu na maombi” Alisema Mch. Ngoda.

Uteuzi wa nafasi ya Mkuu wa Jimbo la Magharibi, ulifanyika katika kikao Maalum kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Utondolo Lushoto-Tanga mnamo, tarehe 15-16/06/2023, Ndipo Halmashauri Kuu ya KKKT -Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ilipitisha jina la Mch. Ishmael Reuben Ngoda kuwa Mkuu wa Jimbo Teule la Magharibi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mwl. Julius Samwel Madiga katika itikio lake mara baada ya kuingizwa kazini na kukubali kupokea wajibu huo amemshukuru Mungu kwa kupata nafasi hiyo ya kutumika shambani mwa Bwana na kuahidi kuitumikia nafasi hiyo kwa maslahi mapana ya Dayosisi.

 “Ninamshukuru Mungu kwa kupitia ninyi pamoja na vyombo mbalimbali vya Dayosisi kwa kunipa wajibu huu adhimu wa kumtumikia Mungu katika Kanisa letu la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa nafasi ya Katibu Mkuu, nafasi ambayo ni kubwa na nyeti sana.”Alisema Mwl. Julius Madiga.

Aidha, Mwl. Julius Madiga ameongeza kwa kuwashukuru kwa dhati Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya KKKT-DKMs chini ya Mwenyekiti wake Mha. Baba Askofu Mch. Dkt. Msafiri Joseph Mbilu na Msaidizi wake Mch. Michael Mlondakweli Kanju kwa kumkubali na kumpokea kwa niaba ya Wanadayosisi kuwa Katibu Mkuu wa Dayosisi huku akiahidi kutoa ushirikiano kwa viongozi wa Dayosisi na Serikali.

“Naahidi kuwa nitatoa ushirikiano mzuri na mkubwa kwa Baba Askofu na Viongozi wengine wote pamoja na waumini wote kwa ujumla wao. ili Dayosisi na Kanisa kwa ujumla tusonge mbele tufike wakati Dayosisi na watu wengine waje wajifunze kwetu na sio sisi kwenda huku na huko kujifunza.”

Wapendwa, natambua kazi nzuri sana zinazofanywa na Serikali yetu. Na pia najua jinsi ambavyo Serikali yetu inavyoshirikiana na Taasisi za Dini likiwemo Kanisa letu la KKKT. Natambua kwamba KKKT-DKMs inafanya kazi kwa karibu sana na Serikali yetu katika Nyanja mbalimbali kama vile Elimu, Afya, Maji na huduma nyingine za kijamii. Jambo hili ni jema sana na niombe tuendelee hivyo hivyo kwani sisi tu wadau wa Serikali na si washindani. ”  

Uteuzi wa nafasi ya Katibu Mkuu wa Dayosisi ulifanyika katika kikao Maalum kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Utondolo Lushoto Tanga mnamo, tarehe 04/11/2022, Ndipo Halmashauri Kuu ya KKKT -Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ilipitisha jina la Mwl. Julius Samwel Madiga kuwa Katibu Mkuu wa Dayosisi akichukuwa nafasi ya mtangulizi wake Mch. Godfrey Tahona Walalaze ambaye alimaliza muda wake.

Safu ya Wakuu wa Majimbo matano (5) ya KKKT-DKMs inaundwa na. Mkuu wa Jimbo la Kusini ,Mch. Issai Mweta (Wa kwanza kutoka kushoto), Mkuu wa Jimbo Mteule wa Jimbo la Pwani, Mch. Emmanuel Mtoi (Wa pili kutoka Kushoto), Mch. Ishmael Reuben Ngoda, Mkuu wa Jimbo la Magharibi (Aliye katikati), Mch. Anderson Kipande Mkuu wa Jimbo la Kaskazini  (Wa kwanza kutoka kulia) na  Mkuu wa Jimbo la Tambarare, Mch. Frank Mtangi (Wa pili kutoka kulia).