Mei 9 mwaka 2021 ilikuwa ni siku iliyotawaliwa na nderemo, vifijo na shamrashamra katika viunga vya Lushoto, siri nyuma ya furaha hii si nyingine bali ni historia mpya kuandikwa, wakristo wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki walipata Askofu mpya, kiongozi ambae atayabeba maono na dira ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki huyu sio mwingine bali ni Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu.Mhadhiri huyo mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Silliman cha nchini Ufilipino, aliingizwa kazini katika Ibada iliyofanyika  Kanisa Kuu Lushoto tarehe 09/05/2021 na kisha yeye kumuingiza kazini msaidizi wake, Mch. Michael Mlondakweli Kanju.

leo tarehe 09/05/2023 zimetimia siku 730, yaani miaka miwili tangu alipoingizwa kazini kushika wadhifa huo , bado tunaiona shauku ileile ndani yake kwani licha ya kusimamia mafundisho ya Neno la Mungu kwa usahihi wake, Askofu Dkt. Mbilu amesimamia msingi wa Dayosisi kumhudumia mwanadamu kimwili, kiakili na kiroho.

Askofu Dkt. Mbilu licha ya kusimamia Dayosisi kupitia kauli mbiu yake ya kasi tofauti, ameendelea kuwa mnyenyekevu na msikivu kwa washarika wote  kwani anaamini ushirikiano mzuri wanaompa ndio msingi wa mafaniko ya Dayosisi pamoja na utekelezaji wa mpango kazi wa miaka mitano wa Dayosisi. mpango kazi huo ni dira, barabara na ramani  ya Dayosisi katika kuonesha muelekeo  wa miaka mitano ijayo. mpango huo umeandaliwa kwa kushirikisha  wadau mbalimbali wa Dayosisi  kuanzia ngazi za chini kabisa hadi za juu.

Kwa upande wake msaidizi  wa Askofu Mch. Michael Kanju amewashukuru wanadayosisi waliopo ndani na nje ya Dayosisi kwa namna walivyo shirikiana na uongozi katika kipindi hiki cha miaka miwili huku akitaja baadhi ya mambo yaliyofanyika ikiwa ni pamoja na.

kufunguliwa kwa taasisi ya elimu ya Kolowa Technical Training Institute (KOTETI), ,kuimarisha utawala bora na mifumo imara ya usimamizi wa fedha, kuimarisha huduma za kijamii kwa kufanya Diakonia na kutoa huduma bora, kuboresha uchumi na maendeleo, ukusanyaji na matumizi bora ya rasilimali. kuimarisha uongozi na utawala bora wa taasisi katika uwajibikaji, ushirikiano, uratibu na utengenezaji wa mtandao imara wa kiutendaji.

Kurugenzi ya Missioni na Uinjilisti ni kurugenzi inayoongozwa na Msaidizi wa Askofu Mch. Michael Kanju ambayo ndio msingi na moyo wa kazi ya utume.

“Wapendwa,  huu siyo wajibu mdogo, kwa kuwa utume huu umekuja kwetu kwa kinywa cha Mungu mwenyewe. lakini jambo lingine kubwa sana kwetu ni jinsi Mungu alivyotuamini sisi kuifanya kazi yake hii. maana sisi ni binadamu tu. nimetumia maneno msingi na moyo kwa sababu, msingi ndipo mahali tunaposimamia  na ni katika msingi  ndipo nyumba  hujengwa  na kusimama imara, moyo kwa sababu, si kazi rahisi hivyo bila moyo huwezi kupata msukumo unaotia nguvu na uwezo wa kufanya.

Pasipo kazi hii kufanyika na watu kumpokea na kumkiri Yesu kuwa Bwana na mwokozi katika maisha yao hakuna uzima katika ulimwengu ujao. hii ndiyo lugha ambayo sisi  wanadamu  tunaweza kuielewa  kwa urahisi  na wepesi zaidi. katika kinywa cha Mungu mwenyewe kwa njia ya bwana wetu Yesu Kristo anasema, “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la baba, na mwana, na roho mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama mimi nipo pamoja  nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari” (math. 28:19-20).

Katika kutimiza wajibu huu mkubwa, kupitia kurugenzi hii,  inatekeleza majukumu yake ya siku kwa siku katika majimbo yake manne ambayo ni:- Jimbo la Kaskazini - Makao Makuu ni Mlalo.Jimbo la Kusini - Makao Makuu ni Soni.jimbo la Tambarare - Makao Makuu ni Korogwe. Jimbo la Pwani - Makao Makuu ni Tanga. Dayosisi ina sharika 65 na eneo la Misioni hivyo kufanya jumla ya sharika 66 zenye jumla ya mitaa 1,451. 

Kurugenzi hii inaweka mkazo zaidi kuhakikisha kwamba neno la Mungu na Sakramenti zinatolewa kwa usahihi katika sharika zote. kwa muda wa miaka miwili kurugenzi hii imefanya mambo mengi. matukio makuu yaliyofanyika ni kama ifuatavyo: Semina na mikutano ya Injili sharikani, ambayo  imesaidia kuwaleta watu kwa Yesu, kuwaimarisha wakristo kiroho na kuwasaidia  kupambana na mafundisho potofu, uinjilisti wa nyumba kwa nyumba, ambao umelenga kurudisha mioyo ya wana Dayosisi waliorudi nyuma.  ziara mbalimbali za kichungaji sharikani na majimboni. ujenzi wa majengo mbalimbali kama nyumba za Ibada na nyumba za watumishi. huduma kwa watumishi wastaafu imeboreshwa ikiwemo pensheni na matibabu. Ibada maalumu pale mtumishi anapostaafu. mafundisho ya uwakili ambayo yamewezesha kuongezeka kwa mapato kwa njia ya sadaka na changizo. kuanzishwa kwa sharika mpya. kuandaa  semina kwa wachungaji. kuandaa semina kwa wakuu wa majimbo wa DKMS na wa DMP ambayo ilidhaminiwa na shirika la umisioni la UEM mnamo mwezi April 2021, Tanga. kuimarisha na kuendeleza uhusiano (Partnership) wa sharika, majimbo na Dayosisi, za ndani na marafiki zetu wa nje

“Nampongeza sana Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu kwa juhudi kubwa ambazo amezifanya katika kipindi hiki cha miaka miwili, tumeona mwanga, kipindi alichoingia kilikuwa kipindi kigumu, ambacho kwakweli kiligubikwa na mambo mengi lakini kubwa ni madeni makubwa yanayo ikabili Dayodidi yetu lakini kwa upeo wake mkubwa na utayari wa moyo na mtu mwenye maono makubwa ya kutaka kufanya mambo makubwa yenye matokeo mazuri, tumeona tukipiga hatua kutoka mahali tulipokuwa, mpaka sasa tunaona mwelekeo mzuri” alisema kaimu Mkurugenzi wa Uchumi na mipango Bw.David Chanyeghea na kuongeza

 “Haikuwa rahisi sana kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo kwa kipindi hiki, lakini kwa utashi wa Baba Askofu tumewekeza kwenye miradi mbalimbali”.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, CPA. Peter John Singano alisema anampongeza Baba Askofu Dkt. Msafiri Mbilu kwa kuwaweka wanadayosisi pamoja na kushirikiana nao katika majukumu mengi ikiwemo kupunguza baadhi ya madeni yanayo ikabili Dayosisi.

“Tunawashukuru pia wanadayosisi kwa kuendelee kushirikiana na Baba Askofu, tunaamini  wataendelea kumpa ushirikiano,  nami kwa niaba ya watumishi wa Ofisi Kuu tunaahidi tutaendelea kumpa ushirikiano” alisema CPA. Singano.