Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch. Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amewashukuru wana KKKT-DKMs pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa namna wanavyo endelea kuchangia deni la Dayosisi na kusaidia kumaliza Deni la CRDB na kupunguza sehemu ya madeni mengine yanayo ikabili Dayosisi.

Askofu Dkt. Mbilu ametoa shukrani hizo leo tarehe 12/02/2023 wakati akitoa salamu zake katika Ibada ya Jumapili iliyofanyika Kanisa Kuu Lushoto ambayo iliongozwa na Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Morogoro Mch. Jacob Mameo Ole Paul.

 Askofu Dkt. Mbilu ameongeza kuwa  ni jambo la kumshukuru Mungu kwa jinsi washarika walivyo ingia kazini kuchangia deni hilo jambo lililoleta   uelewa wa pamoja na kupanga kwa pamoja mambo mbalimbali ya maendeleo katika Dayosisi.

 Amesema  kuwa ni jambo la kumshukuru Mungu sana  kwa namna alivyo waunganisha wana KKKT-DKMs pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo  katika kuchangia deni hilo , Tunawashukuru sana kwa jinsi tunavyoshirikiana katika mambo  yahusuyo Dayosisi yetu kwa sasa.wote tunatambua kuwa uongozi wa sasa uliingia katika kipindi kigumu cha madeni makubwa yapatayo Bilioni 7.5 ni dhahiri kabisa watu wa Mungu wanaelewa ilivyo ngumu kutekeleza shughuli za maendeleo katika Dayosisi yetu wakati tukiwa na madeni makubwa  tena hatarishi.

Deni la Dayosisi ni kubwa lipatalo kiasi cha Bilioni 7.5 kama ilivyoelezwa mwanzoni.Tunamshukuru Mungu sana  kwa washarika kuelewa uwepo wa deni hili, pili kushirikiana kwa pamoja kulilipa,  na kwa awamu hii ya kwanza ya uchangiaji tunakusudia kukusanya kiasi cha Bilioni 1.2 na awamu hii ya kwanza imeongezewa muda wa uchangiaji hadi mwezi Machi 2023 ilikutoa nafasi kwa wale ambao hawakuweza kuchangia kufanya hivyo.

 Hadi sasa deni la Dayosisi limepungua na kufikia kiasi cha Bilioni 6.2 hii Imechangiwa na washarika kushiriki katika ulipaji kupitia harambee  inayoendelea, mipango mbalimbali ya Ofisi Kuu, na msaada wa washirika wetu na wadau wa maendeleo kwa kutuwezesha kupata Mkopo rahisi uliopelekea kumaliza Deni la CRDB na kupunguza sehemu ya madeni mengine.

Askofu Mbilu ameendelea kutoa rai kwa wanadayosisi kushiriki tena kuendelea kulipa Deni hilo  kwani kwa ushiriano wa pamoja deni hili litaisha.

Askofu Dkt. Mbilu alitamatisha salamu zake kwa kuwasihi  na kuwakumbusha wanadayosisi kuwa kuna madeni mengine hatarishi  hivyo ni vyema kuingia kazini katika awamu nyingine na  kutokurudi nyuma katika kuchangia deni hilo kubwa la Dayosisi ilikuendelea kuwalipa wadeni mbalimbali kama vile  TRA,NSSF,watumishi wa kilichokuwa Chuo Kikuu cha SEKOMU huku akiweka wazi kua pamoja na uwepo wa madeni hayo makubwa bado kazi za maendeleo katika Dayosisi zimeendelea kufanyika. Kupitia sadaka ya maendeleo ambayo washarika wameendelea kuitoa  imesaidia kufanikisha utekeleji wa majukumu ya kiutendaji ya kila siku na kuleta maendeleo katika  Dayosisi.