Askofu  wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch.Dkt Msafiri Joseph Mbilu leo Tarehe 25/12/2021 ameongoza Ibada katika Kanisa Kuu (Cathedral) Lushoto.Ikiwa leo ni sikukuu ya Krismas Baba Askofu Mbilu amehubiri neno la Mungu kutoka kitabu cha Luka 2:10 nalo linasema “Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote”.

Sikukuu ya Krismas, ni sikukuu kubwa inayosherehekewa na watu wengi Ulimwenguni pote. Siku hii ni siku ambayo  Wakristo wanapokea zawadi kubwa kutoka kwa Mungu mwenyewe kwa kumtoa mwanawe mpendwa Yesu Kristo azaliwe katika ulimwengu huu kwa ajili ya ukombozi wetu.

Kabla ya kuzaliwa kwa Yesu, watu walikuwa wakingojea kwa hamu kubwa ujio wa Masihi atakayewaokoa kutoka kwenye utumwa dhalimu wa Dunia uliowakandamiza. Yesu anakuja kama jibu la ukombozi wa watu ambao umebeba maana kubwa ya kiroho na siyo ya kisiasa.

Mwinjilisti Luka anaweka wazi tangazo la Malaika kuwa ujio huu ni Habari njema, katikati ya watu waliokuwa wamejawa na hofu kuu. Neno linasema wachungaji wakiwa makondeni katika majukumu yao ya kuchunga na kulinda mifugo yao ghafula waliona utukufu wa Bwana ukiwazukia pande zote. Wakashikwa na hofu kuu.

Ndipo Makaika wa Bwana akaleta ujumbe akiwaambia Msiogope ninakuja na Habari njema. Tena anaweka mkazo akisema kuwa habari njema hii si kwa ajili yenu tu, bali ni kwa watu wote.

Ujumbe huu wa habari njema kwa watu wote ndiyo mkazo mkuu katika sikukuu hii tunapokumbuka kumpokea Mwokozi wa ulimwengu anayezaliwa kwetu.

Katika wakati wa Dunia tunayo ishi sasa,lipo ongezeko la uasi na uovu,anguko la uchumi,hofu ya uharibifu wa mazingira ambao unaleta mabadiliko makubwa ya tabia ya Nchi yanayosababisha ukame mkubwa,Ongezeko la Joto, na mahali pengine mafuriko ya kutisha,hofu ya magonjwa ya kutisha mfano ugonjwa wa Corona (UVIKO -19) na mengineyo yasiyo na tiba

Hofu hizi na nyinginezo  zinazotuzunguka zinatuweka katika hali ya wasiwasi mkubwa, hivyo tangazo la Malaika la kutuondolea hofu linakuja kwa wakati muafaka kwetu sote leo hii.

Habari njema ya furaha kuu inayoletwa kwa watu wote iendelee kuwa nguzo na tumaini letu la kutufanya tutembee kifua mbele, bila hofu huku tukiandaa mioyo yetu ili Mwokozi huyu wa Ulimwengu azaliwe mioyoni mwetu na kugeuza hofu zetu ziwe furaha kuu. Furaha hii iguse watu wote wake kwa waume, Watoto, vijana na wazee.

Furaha hii ituguse sote wana KKKT-DKMs katika kujitoa kwetu tukimtanguliza Mungu afufue kazi zetu, miradi yetu na kuvikuza vituo vyetu ili mwisho wa yote Bwana ajitwalie utukufu.

Heri ya  Krismas