
Mwanamke mwema ni taji la mumewe ;bali aaibishae ni kama kuoza mifupani mwake. Mithali 12: 4 haya yamehubiriwa leo tarehe 26/11/2021 na Mchungaji Sabina Lumwe katika ibada ya ufunguzi wa warsha ya wake wa wachungaji na mashemasi kutoka Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na Dayosisi ya Mashariki na Pwani. ambapo Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ndiye aliyekua mgeni rasmi wa warsha hiyo inayofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa SEKOMU-Lushoto Tanga
Askofu Dkt Msafiri Mbilu wakati wa ufunguzi amesoma neno kutoka kitabu cha Mithali 12:2 na kusisitiza wake wa Wachungaji waendelee kuwa taji kwa kufanya mema na kumcha Mungu sambamba na hilo amewasisitizia kutokujichanganya kwengine bali kukumbuka wao kuwa ni Walutheli.

Hata hivyo baba Askofu amesisitiza utanashati, upole, uaminifu na kutopenda utajiri wa haraka haraka ni vitu muhimu kwa mke wa Mchungaji, mbali na hayo mke wa Mchungaji anapaswa kuwa mchakarikaji na kuwa mpambanaji kwenye suala zima la kuimarisha kipato cha familia.

Warsha hii imeandaliwa na UEM kwa kushirikiana na Dayosisi ya Kaskazini Mashariki pamoja na Dayosisi ya Mashariki na Pwani.
UEM: United Evangelical Mission ni chama Cha kiinjili Cha kimisioni kilichoanzishwa miaka 25 iliyopita na wamisionari kutoka Ujerumani wa Rhenish na Betheli ambao walifika Africa, na Asia kwa ajili ya kuanzisha shughuli za Dini. Katika Africa walifika katika nchi 7 ambazo ni Tanzania, DR Congo, Africa ya Kusini, Botswana, Cameroon, Namibia na Rwanda kukiwa na madhehebu 15. Katika Tanzania inawakilishwa na Makanisa 4 ya KKKT ambayo ni KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani pamoja na KKKT Dayosisi ya Karagwe.

Aidha Chama hiki kinashughulika katika nguzo tano ambazo ni Uhusiano/ Undugu, Diakonia, Uinjilishaji, Utetezi pamoja na Maendeleo.

