Mchungaji Jeremia Mboko wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Jimbo la Pwani Usharika wa Mikanjuni amewashukuru na kuwapongeza waumini wa Usharika huo ambao wanaendelea kujitoa katika kuchangia deni linalo ikabili Dayosisi huku akiwataka washarika wote kuingia kazini kikamilifu katika kuchangia deni hilo.


Mch. Mboko ametoa shukrani hizo kwenye Ibada ya Jumapili ya Terehe 28/04/2024 iliyofanyika katika Usharika huo ambapo aliendelea kuwashukuru Washarika ambao wapo nje ya Usharika huo kwa kuendelea kuchangia deni la Dayosisi. “Ndugu zangu, wapo washarika wenzetu ambao wapo nje ya Usharika wetu ila wanazo bahasha za kuchangia deni na wanazitumia vizuri nina washukuru sana kwa moyo wao wa kujitoa.”Alisema Mch. Mboko ambapo katika Ibada hiyo jumla ya kiasi cha Tsh.729,650 kilipatikana kwaajili ya deni la Dayosisi.
Aidha Mchungaji Mboko ameongeza kwa kusema kuwa wapo baadhi ya washarika ambao hawajaanza kutumia bahasha zao kwa ajili ya kuchangia deni kama ilivyopangwa na uongozi wa Dayosisi kila mwezi msharika kuchangia kiasi cha Tsh. 10,000, hivyo akawasihi washarika hao kuhakikisha kila mmoja anaingia kazini katika kuchangia ili kulipa deni hilo ili viongozi wa Dayosisi waweze kufanya shuguli nyingine za maendeleo.
Katika hatua nyingine Mch. Mboko amehimiza juu ya Uchaguzi wa serikali za Mitaa, huku akiwataka wenye sifa kujitokeza katika uchaguzi wa serikali za Mitaa, kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye Mitaa yao pamoja na kuhuisha taarifa zao katika daftari la Kudumu la Wapigakura ili kuwa na sifa ya kushiriki kwenye uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa unaokuja na baadae uchaguzi Mkuu wa Mwakani 2025.