
Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch. Dkt. Msafi Joseph Mbilu, ameitaka jamii ya wanakijiji wa Gemai kuhakikisha wanalinda na kutunza mradi mkubwa wa maji pamoja na kuendelee kuchangia michango midogomidogo ya kila mwezi ili kuwezesha utunzaji wa miundombinu ya mradi huo.

Ameyasema hayo hapo jana akiwa katika ziara yake ya siku tatu katika Jimbo la Kaskazini Ushaharika Mteule wa Nywelo-Gemai kwenye uzinduzi wa mradi huo ulioko katika Kijiji cha Gemai Kata ya Mkumbara Wilaya ya Korogwe Mko wa Tanga huku akiwashukuru wafadhili kutoka Ujerumani Jimbo la Minden pamoja na Serikali ambao wamewezesha kukamilika kwa mradi huo ambapo kwa sasa hakuna adha ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo.
Baba Askofu Dkt. Mbilu amesema kua KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa kushirikiana na Serikali kwa pamoja wameendelea kuihudumia jamii ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mradi huo wa maji ujulikanao kwa jina la ‘MAZI KWA WOSHE’ ikiimaanisha MAJI KWA WOTE jina ambalo muasisi wake ni Baba Askofu Dkt. Mbilu.
Kwa upande wao wanakijiji wa Gemai wameshukuru sana kuwepo kwa mradi huo na kukamilika kwake na wameupokea kwa furaha kubwa kwani hapo awali walikua wakipata changamoto ya maji kwani walikua wakiyapata kwa umbali mrefu lakini kwasasa mradi huo umesaidia katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji.

Ziara hiyo ya Baba Askofu Dkt. Mbilu iliyotamatika Jumapili ya leo tarehe 23/04/2023 katika Usharika Mteule wa Nywelo, ilikua ni ya siku tatu katika Jimbo hilo ambapo pamoja na ufunguzi wa mradi huo wa maji, kuwatembelea Washarika na kuombanao majumbani kwao pia Baba Askofu amezindua kazi ya Uinjilisti wa nyumba kwa nyumba utakao fanyika katika Sharika na Mitaa yote ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa miezi miwili, huku akiwataka Washarika kuwapokea watumishi wa Mungu punde watakapofikia katika nyumba zao.

