
Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewataka Wakristo kuendelea kukemea vikali vitendo vya ukatili na viashiria vya mapenzi ya jinsia moja katika jamii kwani huo ndio msimamo wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, na Kanisa kwa ujumla.
Askofu Mch Dkt. Mbilu ametoa wito huo wakati akihubiri katika Ibada ya Jumapili ya Pasaka iliyofanyika Kanisa Kuu Lushoto, ambapo amesema kuwa msimamo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na Afrika kwa ujumla haliungi mkono ndoa wala mapenzi ya jinsia moja.

Askofu Dkt. Mbilu amesema hakuna haki za binadamu katika dhambi yoyote ikiwemo mapenzi ya jinisia moja na kuwataka Wakristo kufufuka upya na Yesu Kristo mkombizi wa ulimwengu katika kukemea na kupinga kila aina ya uovu katika jamii.
Amesema kuwa Kanisa likisimama katika maombi na kumtegemea Mungu ataonyesha baraka zake na kufufua kwa upya kazi yake na ndio baraka zitawajilia watu wake na kuuona ukuu wa Mungu katika maisha yao huku akiwataka Washarika na jamii kwa ujumla kufanya mambo yafuatayo 1/ Kutubu mbele za Mungu atuondolee uovu wetu na kutuamsha kwa upya pale tulipoanguka 2/ Kusimama kwa pamoja kukemea dhambi na kuukataa uovu wa kila aina katika jamii 3/ Kumuomba Mungu atuepushe na maovu yanayotanda katika ulimwengu wa sasa.

Katika hatua nyingine Askofu Dkt. Mbilu amewatahadharisha Wakristo kuepukana na mafundisho potofu yenye kupinga kweli ya Kristo na yenye kuwaacha watu wakihangaika katika imani.



Ibada hii ya Jumapili ya Pasaka Imehudhuriwa pia na Askofu Mstaaafu wa KKKT-DKMS Mzee Joseph Jali, Msaidizi wa Askofu Mch. Michael Mlondakweli Kanju, Wachungaji,Wainjilisti, Washarika na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania.


