Print

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amefungua rasmi Mkutano Mkuu  wa 4 baada ya Jubilee ya miaka 125 ya Injili KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, leo tarehe 30/03/2023 katika ukumbi wa mikutano  wa Benjamin William Mkapa Auditorium KOTETI Magamba.

Mkutano Mkuu huu unaongozwa na Neno Kuu la Dayosisi kutoka kitabu cha Ayubu 22:21 lisemalo “ Mjue Sana Mungu, Ili Uwe Na Amani;Ndivyo mema yatakavyokujia”. Kutokana na changamoto kubwa ya mmomonyoko wa maadili na kushamiri kwa tatizo la mapenzi ya Jinsia moja sehemu ya maaskofu waliohudhuria katika mkutano huu wakati wakitoa salamu zao  wamewakumbusha waumini wa Kanisa la KKKT, Wajumbe wa Mkutano Mkuu na Jamii kwa ujumla kukemea vitendo hivyo kwa nguvu na kuomba toba kwa hilo ili kuepukana na ghadhabu ya Mungu.

Aidha wazazi wamekumbushwa kurudi kulea familia na kujenga ukaribu na watoto. Malezi ya siku hizi yamelegea hivyo ni wakati wa wazazi kusimama na kupambana na pepo hili la ushoga ambalo sio hadidhi tena bali lipo katika jamii yetu na ndani ya familia zetu.

Mbali na hayo,Mwakilishi wa Mkuu wa Kanisa, Askofu Chediel Sendoro wa KKKT-Dayosisi ya Mwanga ameupongeza Uongozi wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa kazi nzuri zinazoendelea na pia utulivu uliopo katika Dayosisi na ameongeza kuwa mkutano huu Mkuu ambao ndio chombo cha juu cha maamuzi uwe njia itakayojenga maendeleo zaidi ya Dayosisi na kuendana na kauli mbiu ya KASI YA TOFAUTI.

Mkutano huu umehudhuriwa na mababaaskofu  akiwemo Askofu Chediel Sendoro wa KKKT-Dayosisi ya Mwanga aliyemuwakilisha Mkuu wa Kanisa la KKKT, Askofu Jacob Mameyo wa KKKT-Dayosisi ya Morogoro, Askofu Charles Mjema wa KKKT-Dayosisi ya Pare, Askofu Dkt Syprian Hilinti wa KKKT-Dayosisi ya Kati, Askofu Mstaafu wa KKKT-DKMs Mzee Joseph Jali wageni waalikwa kutoka Taasisi za Kibenki; meneja NMB tawi la Lushoto,meneja CRDB tawi la Lushoto ,Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank,wachungaji wastaafu,wajumbe wa Halmashauri Kuu ya KKKT-DKMs na Wawakilishi wa Washarika wa KKKT-DKMs.

 

Hits: 12553