
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Askofu Dkt. Fedrick O. Shoo ameshuhudia kuwa, kwa huduma mbalimbali za kijamii zinazoendelea kutolewa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ni ishara nzuri inayodhihirisha nafasi yake kama Kanisa katika kufanya huduma za Diakonia ndani ya jamii.

Mkuu huyo wa KKKT ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) amesema kuwa katika vituo mbalimbali alivyotembelea wakati wa ziara yake inayoendelea KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki amekuta watoa huduma wenye furaha na kazi wanayoitenda hali inayodhihirisha kuwa wanayo matumaini licha ya changamoto zinazoikabili Dayosisi.

Askofu Dkt. Shoo amebainisha hayo leo 31/7/2022 wakati akitoa salamu zake kwenye Ibada ya siku ya Bwana ya saba baada ya Utatu aliyoiongoza akiwa kwenye Usharika wa Kanisa Kuu Lushoto.

Mbali na hayo amepongeza ushirikiano mzuri uliopo baina ya viongozi wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao umejidhihirisha kwa vitendo wakati wote wa ziara yake.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Lushoto ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya Mhe. Kalisti Lazaro amesema kuwa Serikali na Kanisa wamekuwa wakishirikiana katika maendeleo kwa muda mrefu na kipekee Dayosisi ya Kaskazini Mashariki imekuwa ikitekeleza wajibu huo kwa kupeleka huduma mbalimbali za maendeleo katika maeneo ambayo wakati mwingine serikali haikufika.

Katika hatua nyingine Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Dkt. Msafiri Joseph Mbilu alimueleza Mkuu wa Kanisa kuwa wanadayosisi ya Kaskazini Mashariki wanajisikia fahari kuwa sehemu ya kazi za umoja wa Kanisa na miongoni mwa wanajumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) hivyo imekuwa ikitoa na kuwasilisha michango yote inayopaswa kufanya hivyo.

