Naye atafuta kila chozi katika macho yao,wala mauti haitakuwepo tena,wala kilio,wala maumivu hayatakuwepo tena, kwa kuwa mambo ya kwanza , yamekwisha kupita UFUNUO 21:4.

Msaidizi wa Askofu KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch. Michael Mlondakweli Kanju leo tarehe 14/04/2022 ameongoza Ibada ya mazishi ya Marehemu Mzee Nicholas Fredrick Mkala ambaye pia ni kaka wa Mch. Lewis Fredrick Shemkala wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Usharika wa Hale.

Ibada imefanyika katika Kitongoji cha Kwamongo,Kijiji cha Kihitu,Kata ya Vuga Jimbo la Bumbuli,Wilaya ya Lushoto Mkoa wa Tanga. Marehemu Mzee Nicholas Fredrick Mkala aliitwa mbinguni Jumatatu ya tarehe 11/04/2022 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alikuwa anapatiwa matibabu.

Kwa niaba ya Uongozi wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki,kupitia kwa msaidizi wa Askofu Mch. Michael Kanju ambaye alimuwakilisha Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki,Mch Dkt Msafiri Mbilu kwenye Ibada hiyo ya mazishi amesema kuwa, Uongozi unatoa pole kwa Familia ya Marehemu, ndugu jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huo mzito. Mungu awape nguvu na faraja ya kweli katika kipindi hiki kigumu. BWANA alitoa, na BWANA ametwaa; jina la BWANA na libarikiwe.





