Print

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, ameipongeza Idara ya Wanawake na Watoto kwa  mipango mizuri iliyojiwekea katika mwaka  wa wanawake 2022 ambapo amesema kuwa endapo itasimamiwa kwa umakini italeta tija kwenye Idara hiyo na Dayosisi kwa Ujumla.

Pongezi hizo amezitoa   tarehe 06/03/2022 kwenye uzinduzi wa mwaka wa Wanawake 2022, KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki wenye kauli mbiu ‘Amka, amka, Debora; amka, amka, imba wimbo’ uliofanyika katika Usharika wa Korogwe Jimbo la Tambarare.

Amewaahidi Wanawake hao ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wanaume wa KKKT-DKMs. Hata hivyo Askofu Dkt Mbilu hakusita kuwashukuru Wachungaji wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa kuonyesha moyo wa kujitoa na kuingia kazini kwaajili ya kuchangia madeni yanayoikabili Dayosisi, katika kikao maalum cha Askofu na Wachungaji kilichofanyika tarehe 04/03/2022 Kanisa Kuu Lushoto jumla ya Milioni 24 ilipatikana hii ikiwa ni ahadi na pesa taslimu.

Ameyaalika makundi mengine yakiwemo ya wakina mama,vijana na wadau wa maendeleo waliopo ndani na nje ya Dayosisi kuingia kazini punde watakapo pokea barua juu ya namna ya kuchangia madeni hayo ambapo kwa ujumla deni lote la Dayosisi ni  zaidi ya Tsh7,000,000,000.  Bilioni saba likiwepo deni la CRDB, NSSF, TRA, Watumishi wa vituo mbalimbali, kesi na sehemu nyingine. Katika awamu hii ya miezi 6 uongozi unatazamia kukusanya  kiasi cha Tsh. 3,000,000,000 Bilioni tatu.  

Idara ya Jinsia na Watoto ni miongoni mwa Idara muhimu ndani ya KKKT-DKMs ambayo inahudumia kitengo cha Wanawake,Watoto na Wanaume ikiwa na jumla ya wanawake 30,150 kutoka katika majimbo manne ambayo ni Jimbo la Kaskazini wanawake 4914, Jimbo la Pwani 5765, Jimbo la Kusini 869 pamoja na Jimbo la Tambarare wapo wanawake 11,135.

 

Kwa niaba ya Wanawake hao Mratibu wa Idara ya Jinsia na Watoto KKKT-DKMs Mch Happiness Diu hakusita kuishukuru Halmashauri Kuu ya KKKT-DKMs ambayo kupitia kikao chake cha tarehe 9-10/12/2021 kilipitisha na kuamua kuwa mwaka 2022 uwe mwaka wa wanawake  na kuahidi utakuwa na muonekano wa kipekee.

Ameongeza kuwa miongoni mwa malengo mahususi ni kuwajengea wanawake uwezo wa kujiamini na kutumia vipawa walivyonavyo ndani ya Kanisa na jamii inayowazunguka kuimarisha uchumi wa Wanawake ndani ya Kanisa na familia, kuimarisha uchumi wa kitengo cha Wanawake na Watoto, kuwapa Wanawake stadi za uongozi, Wanawake kufanya huduma za kiroho.Hata hivyo ili kutimiza malengo hayo mahususi kutaandaliwa semena za neno la Mungu, malezi, ndoa, haki za Wanawake, ujasiriamali na uongozi, kufanya ziara za kujifunza ndani na nje ya Dayosisi.


Shukrani zimetolewa kwa Uongozi mzima wa KKKT-DKMs, Sharika na Mitaa kwa kuipamba vyema siku hiyo na kipekee kwa wanawake wote ambao hata katika changamoto mbalimbali hawakukata tamaa waliendelea kumtumikia Mungu kwa uaminifu mkubwa kwakuwa wanawake wamtegemeao Bwana ni jeshi kubwa Zab 68:11.

Mkurugenzi wa Kurugenzi  ya Wanawake na Watoto wa KKKT, Bi.Faustina Nillan
Kwa upande mwingine Mkurugenzi wa kurugenzi ya Wanawake na Watoto  KKKT, Bi, Faustina Nillan ametoa shukrani za dhati kwa uongozi wa KKKT-DKMs na kumuomba Askofu Dkt Mbilu kufikisha shukrani hizo kwa Mkuu wa KKKT na Mwenyekiti wa CCT Askofu Dkt. Fredrick Shoo kwa Kanisa kuwaheshimu na kuwathamini Wanawake kupitia KKKT-DKMs kwa kuhakikisha kwamba Wanawake wanapewa nafasi ya kuwa na mwaka wao.


Ameongeza kuwa kwa niaba ya Wanawake wote wa KKKT anaushukuru uongozi wote kwa kuonyesha mfano kwa kutambua  na kuthamini mchango wa Wanawake katika Kanisa na jamii kwa ujumla, amewaasa wanawake kuwa nuru ya kuangaza na kuwa mstari wa mbele katika kazi ya Bwana  kutiana moyo, kuinuana, kupendana pamoja na kufurahiana.

Hits: 15925