Print

Zoezi la kuchangia damu lililo andaliwa na kituo  cha redio Utume Fm kinachomilikiwa na KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kimefanikiwa kukusanya chupa 25 katika Wilaya ya Lushoto mjini.
Hili linajiri wakati ambapo upungufu unashuhudiwa katika benki ya damu Wilayani Lushoto.


Zoezi hilo lilikuwa sehemu ya kampeni ya Onesha Upendo kwa Vitendo lilifanyika 4/3/2022 katika eneo la soko kuu la Wilaya ya Lushoto na kuratibiwa na madaktari kutoka Hospitali ya Wilaya ya Lushoto.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Bi. Evelyn Balozi ambae ni kaimu meneja wa redio Utume amewashukuru wakazi wa Lushoto mjini kwa uamuzi wa kuchangia uhai wao kupitia damu walizochangia.
Aidha amemshukuru Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Ikupa Harison Mwasyoge kupitia Hospitali ya Wilaya ya Lushoto kwa kuridhia kuungana na watumishi hao wa redio Utume na wadau wake wengine kufanikisha kampeni hiyo.
Kwa upande wake Dkt Mohamed Almasi amefurahishwa na kampeni hiyo na ameitaja kama tukio kubwa sana lililofanywa na Utume FM Radio na alishauri isiwe  mwisho wa kampeni kama hiyo kwasababu uhitaji ni mkubwa sana na chupa moja ya damu inaokoa uhai wa mtu anayehitaji.


Kampeni ya Onesha Upendo kwa vitendo imeendeshwa kwa siku 31 kuanzia Februari Mosi hadi Machi 3, mwaka huu ikiambata na utoaji wa elimu kuhusu dhana ya upendo kuanzia ngazi ya familia hadi jamii, kuhamasisha masuala ya Diakonia, kushiriki zoezi la uchangiaji damu salama ambapo wamepokea muitikio mkubwa kutoka kwa jamii na baadhi ya watu walijitolea kuleta nguo, mchele, sukari, sabuni pamoja na fedha taslimu.
Mahitaji yaliyopatikana kwenye kampeni hiyo yatapelekwa kwenye vituo vya wahitaji vya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki,Serikali pamoja na kwenye jamii hasa wale wanayoishi kwenye kaya masikini.

Hits: 14510