Print

Askofu Mstaafu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mzee Joseph Jali ametoa wito kwa wana KKKT-DKMs,ndugu, jamaa na marafiki waliopo ndani na nje ya Dayosisi kuingia kazini ili kukamilisha ujenzi wa bwalo la chakula katika shule ya Bangala Lutheran Junior Seminary ulio simama kwa takribuni miaka 20.

 

Wito huo ameutoa jana tarehe 24/01/2022 alipotembelea shule hiyo pamoja na uongozi wa KKKT-DKMs. Mzee Jali ameongeza kuwa anatambua mwaka huu ni mwaka wa wanawake katika Dayosisi hivyo anawaalika wanawake wa KKKT-DKMs kuungana nae katika ujenzi wa bwalo hilo.

Ikumbukwe kuwa mnamo tarehe 19/11/2021 yalifanyika maadhimisho ya miaka 60 ya ndoa yake katika Kanisa Kuu Lushoto na kiasi cha pesa kilichopatikani katika maadhimisho hayo alikielekeza katika ujenzi wa bwalo kama sehemu ya mchango wake.

Kwa upande mwingine Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amesema kuwa kwa takribani miaka 20 ujenzi wa bwalo hilo haukupewa kipaombele lakini sasa uongozi unaanza kwa upya na kazi itafanywa na wana Dayosisi kwa nguvu kubwa.

Ameongeza kuwa gharama za ujenzi wa bwalo hilo zitawekwa wazi ili kutoa fursa kwa wana Dayosisi pamoja na marafiki waliopo ndani na nje ya Dayosisi kuona ni kwa namna gani wanaweza kushiriki kuchangia ujenzi huo.

Hata hivyo Askofu Dkt Mbilu ametoa maelekezo ya ujenzi huo kuanza mara moja kwakuwa kuna kiasi cha pesa kilichotolewa na Askofu Mstaafu Mzee Jali kama sehemu ya mchango wa bwalo hilo.

Hits: 15019