
Msaidizi wa Askofu KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch. Michael Mlondakweli Kanju ameupongeza uongozi wa kituo cha Redio Utume Fm chini ya Kaimu meneja wa kituo hicho Bi. Evelyne Balozi Mariki kwa kuendeleza maono ya Dayosisi ya kueneza Injili kwa wote.
Pongezi hizo amezitoa leo Novemba 19, 2021 wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Maombi na Maombezi lililofanyika katika Usharika wa Gombero, senta ya Usharika. Kongamano hilo limeandaliwa na kituo cha Redio Utume kwa siku tatu Novemba 19 hadi 21 mwaka huu kupitia kipindi chake cha Ita naye ataitika kinacho ruka kila siku ya jumapili kuanzia saa nne kamili usiku hadi saa kumi alfajiri.

Timu ya Redio Utume wameshirikiana na watumishi wa Mungu, Wachungaji John Ndimbo na Warehema Chamshama, Mwinjilisti Yohana Kolowa, Mtheolojia Justine Mhombo pamoja na Mchungaji mwenyeji Johnson Pokeaeli.

Aidha msaidizi wa Askofu ameupongeza Usharika wa Gombero unaoongozwa na Mch. Pokeaeli kwa kukubali kupokea jukumu la kushirikiana na Redio Utume Fm kuandaa na kufanikisha kongamano hilo.

Pamoja na hayo Msaidizi wa Askofu ametoa wito kwa wanadayosisi kuingia kazini kwa matoleo na sadaka tarehe 28/11/2021 ili kuunga mkono maono ya Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu ya kukiwezesha kituo cha Redio Utume FM kuongeza usikivu ili kusikika katika maeneo mbalimbali na kuanzisha vyombo vingine vya Habari ambavyo ni Gaazeti la Utume na Televisheni.

