Print
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch.Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amehitimisha ziara yake ya siku tatu ya kutembelea Jimbo la Pwani na Sharika zake kwa kuongoza Ibada ya Jumapili katika Usharika wa Maramba katika Jimbo la Pwani.
Katika Ibada hii Askofu Dkt. Mbilu ametoa wito kwa Washarika wa Maramba na Dayosisi kwa ujumla kutokubali kupotoshwa na watu wanaosema Dayosisi haidaiwi na badala yake waendelee kuifanya kazi ya Mungu kwa Moyo ikiwemo kuweka juhudi katika kuchangia na kumaliza Deni la Dayosisi.
Awali akiwasili katika usharika wa Maramba Askofu Dkt Msafiri Mbilu alikagua ujenzi wa Hosteli ya kisasa inayojengwa na Usharika huo ikiwa na vyumba kumi na chumba kimoja maalumu cha Viongozi ambapo Askofu Dkt. Mbilu ameunga mkono juhudi za kumalizia ujenzi kwa mchango wa Shilingi milioni moja.
Katika Ziara yake Askofu Dkt.Mbilu amewakumbusha Wakristo kuendelea kuwa mawakili wazuri katika kutunza mazingira kwa kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia Nchi na kupunguza Hewa Ukaa ambayo ni hatari kwa viumbe hai.
Katika siku tatu za Ziara hii Askofu Dkt.Mbilu alitembelea Misioni ya Mjesani,Usharika mteule wa Mapatano,Usharika Mteule wa Lugongo na Usharika wa Maramba akiambatana na Msaidizi wake Mch. Michael Mlondakweli Kanju,Mkuu wa Jimbo la Pwani Mch.Frank Mtangi na aliyekua kaimu Mkuu wa Jimbo la Pwani Mchungaji mstaafu Emmanuel Mtoi.
Hits: 702