Print

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewataka Wakristo kumpokea Yesu na kumkaribisha mioyoni mwao ili afanyike Nuru katika maisha yao na kuondoa giza na matendo yasiyofaa ambayo ni chukizo mbele za Mungu yaliyo tanda  katika ulimwengu na kuwasihi kumpokea  Yesu Kristo ambaye  ni  nuru ya ulimwengu.

 

Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo katika Ibada ya kukumbuka kuzaliwa kwamwokozi  Yesu Kristo iliyofanyika katika Usharika wa Kanisa Kuu Lushoto Tanga ambapo amesema kuwa dunia imejaa maovu  mengi  ikiwemo mauaji, maafa na maangamizi mengi na kuwata Wakristo kuitumia sikukuu hii kufanya upatanisho kwa njia ya kumpokea  Yesu Kristo.

Aidha katika Ibada hiyo,Askofu Mstaafu wa KKKT-DKMs Mch. Joseph Jali ametoa kiasi cha Tsh.1,000,000 kwaajili ya ununuzi wa tarumbeta moja ambapo mara baada ya kuungwa mkono na Washarika wengine ambao walitoa ahadi ya kununua   tarumbeta 7 na hivyo  kupatikana  tarumbeta nane zitakazo tumika katika Usharika wa Kanisa Kuu Lushoto.

Mstaafu Jali ameweka alama kubwa na kupitia alama hiyo amefundisha Wakristo jinsi ya kuweka nia katika kila jambo,kwani yeye aliweza kuhifadhi fedha hizo alizopatiwa kama zawadi kwenye kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa iliyofanyika mwaka jana na kukabithi kiasi hicho leo tarehe 25/12/2023.

SEHEMU YA SALAMU  ZA KRISMAS KUTOKA KWA BABA ASKOFU DKT. MSAFIRI JOSEPH MBILU.

"Tazama, bikira atachukua mimba naye atazaa mwana; nao watamwita jina lake Imanuel; yaani, Mungu pamoja nasi"

Wapendwa katika Bwana "Heri ya Krismas"

Siku ya leo ni siku kubwa ya kutimia kwa maandiko na unabii huu wa Nabii Isaya. Katikati ya giza nene la watu kutengwa na Mungu kwa ajili ya anguko lao katika dhambi, Mungu anaamua kufanyika mwili katika mwana wake Yesu Kristo.

Mungu huyu ambaye alikuwa mbali nasi, sasa anaamua kuwa katikati yetu na kuishi nasi - Imanuel - Mungu pamoja nasi.

Uwepo wa Mungu katikati yetu ndiyo nguvu yetu na tumaini letu tunapoishi katika ulimwengu huu uliojaa dhiki nyingi. Tunapotazama ulimwengu uliojaa vita, mauaji, maafa na maangamizi mengi tunaweza kukata tamaa. Lakini kwa njia ya Imanuel tunaona uwepo wa Mungu akiwa katikati yetu.

Tuandae maisha yetu kumpokea Yesu Kristo anayezaliwa leo ili kupitia uwepo wake katika maisha yetu tuendelee kuona uwepo wa Mungu katika maisha yetu.

 

Hits: 2521