ELCT North Eastern Diocese
Askofu Dkt. Mbilu Akabidhi Gari 1 kwa Kituo Cha Lutindi Mental Hospital
- Details



- Hits: 255
ELCT-NED FAMILY BONANZA 2025
- Details

ELCT-NED FAMILY BONANZA, lililoratibiwa na Kurugenzi ya Uchumi, Mipango na Maendeleo Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania – Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs), limefanyika tarehe 13 Desemba 2025 katika Hoteli ya Mbuyukenda, jijini Tanga, likiwakutanisha waumini, wadau mbalimbali pamoja na familia zao kutoka maeneo mbalimbali.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi wa Uchumi, Mipango na Maendeleo wa KKKT-DKMs, Bi. Pendo Lauwo, aliwashukuru kwa dhati washiriki wote waliojitokeza kushiriki Bonanza hilo pamoja na wadau waliotoa michango yao, akisisitiza kuwa mshikamano na moyo wa kujitolea uliooneshwa ni kielelezo cha umoja wa kitaifa katika kulijenga kanisa na jamii kwa ujumla. Alibainisha kuwa mafanikio ya Bonanza hilo yametokana na ushirikiano wa pamoja kati ya kanisa, wadau na jamii.
Bonanza hilo lililenga kuimarisha umoja, ushirikiano na mshikamano wa kifamilia, sambamba na kukusanya fedha zitakazotumika kufanikisha KKKT-DKMs Marathon inayotarajiwa kufanyika mwaka 2026. Aidha, sehemu ya mapato yaliyopatikana yameelekezwa kusaidia watoto wenye mahitaji maalum, hususan watoto wenye changamoto ya usonji (Autism), kupitia ununuzi wa vifaa vya Physiotherapy (tiba ya viungo) kwa ajili ya Kituo cha Irente Rainbow School.
Kupitia tukio hili, Kanisa limeonesha kwa vitendo dhamira yake ya kushiriki katika maendeleo ya kijamii, likisisitiza umuhimu wa upendo, huruma na mshikamano wa kitaifa katika kuwajali watoto wenye mahitaji maalum, ambao ni sehemu muhimu ya jamii na rasilimali ya Taifa.
Kwa upande wake, Mgeni Rasmi wa tukio hilo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Tanga, Bi. Angela Henry Mono, ametoa wito kwa jamii kuendelea kuwajali na kuwaunga mkono watoto wenye mahitaji maalum, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha watoto hao wanapata haki, ulinzi na fursa sawa za maendeleo.
Bi. Mono alieleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za dini, hususan KKKT-DKMs, katika kufikia na kuboresha ustawi wa watoto wenye mahitaji maalum nchini. Aidha, aliipongeza Dayosisi kwa kazi kubwa na ya mfano inayofanya ya kuwahudumia makundi yenye uhitaji, akibainisha kuwa mchango wa kanisa unaunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha ustawi wa jamii na maendeleo jumuishi ya Taifa.

- Hits: 323
Askofu Dkt. Mbilu Atamatisha Kalenda ya Matukio 2025, Awashukuru Wanadayosisi kwa Ushirikiano wa Kipekee
- Details
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs), Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amewashukuru kwa dhati wanadayosisi wote kwa namna wanavyoendelea kujitoa katika ulipaji wa Deni la Dayosisi, akisisitiza kuwa hatua hiyo imekuwa ikitoa matumaini makubwa katika kufanikisha mpango wa kulimaliza deni hilo.
Askofu Dkt. Mbilu ametoa shukrani hizo katika Ibada ya Jumapili iliyofanyika tarehe 07 Desemba 2025 katika Usharika wa Kanisa Kuu Lushoto, ibada iliyoambatana na matukio mbalimbali muhimu ya kiimani na kiuongozi. Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na kubarikiwa kwa Vijana wa Kipaimara pamoja na kuwaingiza kazini Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya KKKT–DKMs.
Aidha, Askofu Dkt. Mbilu alisisitiza kuwa njia madhubuti ya kukabiliana na changamoto ya deni ni kila msharika na kila usharika kutimiza wajibu wake wa kuchangia Deni la Dayosisi kama walivyopangiwa huku akibainisha kuwa utayari wa washarika na wadau wa maendeleo ni ishara njema ya umoja na uwajibikaji katika kulikabili Deni hilo huku akimpongeza MCH. ANNA TULLO MSISILI pamoja na Washarika wa Usharika wa Ubiri ambao wao wamemaliza kiwango chao cha uchangiaji wa Deni la Dayosisi.
Katika hatua nyingine, Askofu Dkt. Mbilu alifunga rasmi kalenda ya matukio ya Dayosisi kwa mwaka huu, huku akitoa shukrani kwa viongozi wa Kanisa, sharika zote, vituo vya kazi na waumini kwa ushirikiano mkubwa waliompatia katika ziara zake ndani na nje ya Dayosisi.
Katika Ibada hiyo, jumla ya Vijana 34 walibarikiwa, huku 2 kati yao wakibatizwa. Kwa kuunga mkono jitihada za Dayosisi katika kulipia deni, vijana hao pamoja na wazazi, walezi na waumini walioshiriki katika Ibada hiyo walitoa mchango wa jumla ya Tsh. 1,411,300.

- Hits: 616
Kikao cha Halmashauri ya Kurugenzi ya Huduma za Jamii KKKT-DKMs
- Details
![]()
Kikao cha Halmashauri ya Kurugenzi ya Huduma za Jamii – KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kimefanyika tarehe 05 Desemba 2025 katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Utondolo, Lushoto.
Kikao hiki kimeonesha kwa namna ya pekee jinsi Kurugenzi hii inavyotekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kusimamia kwa weledi vituo mbalimbali vya huduma ambavyo vimeendelea kuleta manufaa makubwa kwa Kanisa na kwa jamii ya Watanzania kwa ujumla.
Katika kikao hicho, wajumbe walijadili kwa kina mikakati ya kuboresha na kukuza huduma katika vituo vyote vilivyo chini ya Dayosisi. Mkurugenzi wa Huduma za Jamii, Mwl. Afizai Vuliva, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Kurugenzi kwa lengo la kupokea ushauri na maoni ya wajumbe. Taarifa hiyo imeonesha hatua kubwa zilizopigwa, changamoto zilizopo, pamoja na maeneo yanayohitaji kuimarishwa ili kuongeza tija na ubora wa huduma kwa Kanisa na jamii kwa ujumla. Kurugenzi ya Huduma za Jamii inasimamia na kuratibu idara muhimu zinazogusa maisha ya Kanisa na Jamii moja kwa moja, zikiwemo:
- Idara ya Elimu
- Idara ya Afya
- Idara ya Jinsia na Watoto
- Diakonia (Huduma za Uangalizi na Uchangiaji kwa Jamii)
- Idara ya Vijana na UKWATA
Kupitia usimamizi makini wa Kurugenzi hii, vituo hivi vya huduma vya Dayosisi vimeendelea kuimarika na kutoa huduma zenye kiwango bora, hivyo kuifanya KKKT – Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kuwa mfano wa kuigwa katika utoaji na usimamizi wa huduma za kijamii.
Tufuatilie kwenye mitandao yetu ya kijamii
INSTAGRAM - / elctned
FACEBOOK ACCOUNT North Eastern Diocese
FACEBOOK PAGE - ELCT-North Eastern Diocese
YOUTUBE - / KKKT DKMS Online TV
WEBSITE: www.elctned.org
KWA MAONI NA USHAURI:
Simu : +255 743 399 798
- Hits: 801
Page 1 of 133

